Akana njama ya kumuua Mugabe

Image caption Makamu wa Rais Joyce Mujuru

Makamu wa Rais nchini Zimbabwe, anasema anapanga kuchukua hatua za kisheria dhidi ya shirika la habari la kitaifa kwa kumhusisha na njama ya kumuua Rais Robert Mugabe.

Joyce Mujuru amesema amewaamuru mawakili wake kumrejeshea hadhi yake ya kisiasa baada ya kuhusishwa na madai hayo ya uhaini pamoja na ufisadi.

Jarida la Sunday Mail la nchini humo, limeripoti kuwa kuna njama ya kumkodi mamluki kumuua Mugabe ili Bi Mujuru achukue mamlaka.

Mwezi jana Bwana Mugabe alifikisha miaka 90 na kusema hana nia ya kuachia madaraka.

Ametawala Zimbabwe tangu nchi hio kujipatia uhuru mwaka 1980.

'Ushetani'

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Rais Mugabe akiwa na mkewe Grace Mugabe

Rais Mugabe na Bi Mujuru walikuwa wandani wa karibui lakini kwa sasa wamehasimiana huku mjadala wa kumrithi Mugabe ukitokota katika chama tawala cha Zanu-PF kikijiandaa kwa kongamano lake la kitaifa mwezi ujao.

Mkewe Bwana Mugabe, Grace Mugabe amekuwa akiendesha kampeini dhidi ya Bi Mujuru akimtaka astaafu.

Amemtuhumu Bi Mujuru kwa kuwa mtu wa kishetani na mwenye kugawanya watu pamoja na kujipatia pesa kwa njia ya udanganiyifu, kutoka kwa makampuni.

Taarifa ya bi Mujuru akikana madai ya njama hiyo haikutarajiwa.

Ingawa hajaonyesha dalili za kuachia ngazi, anakabiliwa na shinikizo kali sana za kisiasa.

Jarida la Sunday mail liliripoti taarifa hizo za kushtua kwamba bi Mujuru na washirika wake wanapanga kumkodi mamluki ambaye atamuua Mugabe ili achukue mamlaka.

"ninakanusha madai hayo ya uhaini na ufisadi pamoja na kutumia vibaya mamlaka yangu, madai ambayo yamekuwa yakitolewa dhidi yangu kwa mda mrefu sasa,'' alisema Mujuru.

Amewataka mawakili wake kuchukua hatua za haraka za kisheria dhidi ya waliotoa madai hayo na kumharibia sifa yake.