Wakamatwa kwa kumvua nguo mwanamke Kenya

Image caption Wanawake mjini Nairobi waliandamana kupinga kisa ncha kumvua nguo mwanamke kwa kuvalia nguo fupi

Polisi mjini Nairobi wamewakamata watu 100 katika msako baada ya mwanamke mwingine kuvuliwa nguo katika mtaa wa mabanda wa Kayole mjini Nairobi.

Inadaiwa mwanamke huyo alikuwa amevalia nguo zisizo za heshima.

Naibu kamanda wa polisi mjini Nairobi Moses Ombati, amaenukuliwa akisema wengi wa waliokamatwa walikuwa wanaume walevi.

Bwana Ombati aliongeza kusema kwamba, mwanamke huyo alishambuliwa katika mtaa wa Kayole Jumatatu jioni na kwamba polisi wanaendelea na msako.

Mnamo Jumatatu mamia ya wanawake waliandamana katika barabara za katikati mwa mji kulaani kitendo cha kumvua nguo mwanamke mwingine mapema mwezi huu mjini Nairobi.

Wanawake hao waliandamana kufuatia wito kwenye mitandao ya kijamii chini ya kauli mbiu #MyDressMyChoice yaani vazi langu uamuzi wangu au nitavaa nitakachojiamulia mwenyewe.

Waandamanaji hao wakiwemo wanawake mashuhuri, wanasiasa na wanaharakati waliandamana hadi katika kituo cha mabasi ambako mwanamke wa kwanza alidaiwa kuvuliwa mavazi yake kwa madai alikuwa amevalia 'Mini Skirt'