Kasi kutafuta mwafaka kuhusu Nuklia

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Iran inasisitiza inatumia nuklia yake kwa maslahi ya wananchi

Mataifa sita yenye nguvu duniani na Iran yanakutana leo Vienna kwa awamu ya mwisho ya majadiliano kabla ya muda wa mwisho yaliojipa ya tarehe 24 Novemba kufikia makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Lakini bado kuna tofauti kubwa kuhusu mustakabali wa mpango huo wa urutubishaji madini ya Uranium wa Iran na muda wa kuondoshwa kwa vikwazo dhidi ya nchi hiyo.

Iran na mataifa 6 yenye nguvu duniani yana chini ya muda wa wiki moja kutatua mzozo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Mzozo huo umedumu kwa zaidi ya muongo mmoja na umezusha hofu ya vita vipya vya eneo la mashariki ya kati.

Nchi hizo sita zenyw ushawishi zinataka kuhakikisha kwamba Iran haiwezi kutengeneza bomu la nyuklia kwa haraka. Zinaitaka ipunguze urutubishaji wake wa madini ya Uranium. Iran inasema mpango wake ni wa amani na unapaswa kuendelea.

Inataka isitishiwe vikwazo vilivyouathiri uchumi wake. Pande hizo zinashirikiana zaidi ikilingianishwa na miaka ya nyuma lakini bado kuna mapengo, na baadhi ya waangalizi wanaona muda zaidi huenda ukahitajika.