Polisi hawarekodi makosa ya jinai UK

Haki miliki ya picha PA
Image caption Waathirika hupoteza imani dhidi ya vyombo vya kisheria kwa kuwa maamuzi hufanywa na Polisi bila kuwashirikishwa

Zaidi ya robo ya visa vya unyanyasaji wa kijinsia vinavyoripotiwa havirekodiwi na Polisi nchini Uingereza, waangalizi wameeleza.

Chombo huru kinachoangalia utendaji wa Polisi nchini humo kimesema zaidi ya matukio 80,000 kati ya yanayoripotiwa hayarekodiwi na Polisi kila mwaka.

Waziri wa mambo ya ndani,Theresa May haungi mkono utafiti huu,lakini Polisi wamesema hali sasa imeimarika tangu baada ya ripoti hiyo kutolewa.

Uchunguzi ambao uliangalia Ripoti zaidi ya 8,000 zinazohusu uhalifu zilizoripotiwa nchini Uingereza na Wales kati ya mwezi Novemba mwaka 2012 na Oktoba mwaka 2013, ulibaini kuwa visa 37 vya ubakaji havikurekodiwa kuwa makosa ya jinai.

Polisi wana wajibu wa kuwapa taarifa waathirika kutokana na maamuzi wanayoyafikia,lakini katika visa zaidi ya 800 vilivyofanyiwa uchunguzi hakukuwa na rekodi yeyote ambayo ilionesha kuwa waathiriwa hawakupewa taarifa.

Bi May amesema kitendo cha kutorekodi matukio ya uhalifu hakikubaliki kwa kuwa hatua hiyo huwavunja moyo waathirika.

Waziri kivuli wa masuala ya Sera Jack Dromey amesema sasa ni wakati kwa May kufanya mabadiliko kuhusu namna polisi wanavyorekodi matukio ya uhalifu.

Polisi imesema kuwa changamoto hizo zinatokana na kazi nyingi wanazokuwa nazo,tamaduni,changamoto ya maamuzi ya kiutaalamu dhidi ya maslahi ya waathirika,kutokuwa na ufahamu kuhusu taratibu za kurekodi matukio na usimamizi legelege huchangia kwa kiasi kikubwa kutorekodi matukio ya uhalifu inavyopaswa.