Mrembo na dadake wauawa Honduras

Wanaume wawili wamekamatwa baada ya binti mmoja mshindi wa mashindano ya urembo Maria Jose Alvarado,mwenye umri wa miaka 19 pamoja na dadake kupatikana wakiwa wamefariki karibu wiki moja baada ya kutoweka.

Bi Alvarado na dadake Sofia Trinidad, 23, walitoweka Alhamisi baada ya kuonekana wakitoka kwenye karamu karibu na mji wa Santa Barbara.

Alitarajiwa kushiriki mashindano ya urembo ya Miss World mjini London.

Plutarco Ruiz, mtu aliyesemekena kuwa mpenzi wa mwanamke huyo alikamatwa pamoja na mwanamume mwingine kama washukiwa wa mauaji ya wawili hao.

Polisi walinasa silaha na gari, huku mshukiwa mmoja muhimu akitoa taarifa muhimu kwa polisi.

Wanawake hao wawili walionekana mwisho wakiwa hai ndani ya gari iliyokuwa haina leseni wala nambari ya usajiji walioondoka kutoka karamuni Novemba 13.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, wanaume hao waliokamatwa wanaaminika kuwa watu wa mwisho kuwaona wasichana hao kabla ya kutoweka kwao.

''Wawili hao wanahojiwa kuhusiana na uchunguzi kuhusu kutoweka kwa mrembo huyo na dadake, ''alisema msemaji wa polisi Jose Coello.

"tunataka kujua walivyohusika na mauaji hayo,'' alidokeza polisi huyo.

Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa, Honduras ni moja ya mataifa duniani yenye visa vingi vya mauaji