Eritrea:Vijana walazimishwa kuingia jeshini

Image caption Rais wa Eritrea, Isaias Afewerki

Mpango wa kuwasajili Vijana katika Jeshi nchini Eritrea umesababisha kukimbia nchi hiyo kwenda nchi jirani ya Ethiopia, Shirika la linalohudumia Wakimbizi duniani, UNHCR limeeleza.

Zaidi ya Watu 6,000 raia wa Eritrea wameomba hifadhi nchini Ethiopia kwa kipindi cha siku 37 zilizopita, ikiwa ni mara mbili ya waliokimbia miezi iliyopita, msemaji wa shirika hilo Karin Gruijl ameiambia BBC.

Pia idadi ya raia wa Eritrea wanaotafuta hifadhi nchini Italia imeongezeka.

Takriban watu 100,000 walipoteza maisha katika mapambano ya mpakani kati ya nchi hizo mwaka 1988-2000.

Eritrea ilipata uhuru baada ya kujitenga na Ethiopia.

Msemaji wa UNHCR ameiambia BBC kuwa Wakimbizi, wengi wao wakiwa kati ya miaka 18 na 24, wameripoti uwepo wa zoezi la kulazimishwa kujiunga na Jeshi.

Zoezi hili limejenga hofu miongoni mwa vijana hao ambao hawafahamu kuwa hata wakiingia kwenye jeshi watalitumikia kwa muda gani.

Serikali ya Rais wa Eritrea, Isaias Afewerki imekosolewa mara kwa mara na wanaharakati wa haki za binaadamu, ambao wanasema Eritrea ni moja ya nchi duniani zinazokandamiza haki za binaadamu.