Msichana kutoka Syria ashitakiwa

Haki miliki ya picha l
Image caption Monique akiwa mbele ya TV akiomba binti yake kurejea nyumbani Uholanzi miezi miwili iliyopita

Msichana wa kiholanzi aliyerejea kutoka Syria ambako alikwenda huko kujiunga na wapiganaji wa jihadi lakini baadaye alirudishwa nyumbani na mamake anatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa kushukiwa kutishia usalama wa taifa.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka 19, akijulikana kama Aicha, alikamatwa aliporejea nyumbani kwao katika mji wa Maastricht.

Aicha, aliyebadili dini hivi karibuni kuwa Mwislam, anaaminika kusafiri kwenda kujiunga na wapiganaji wa Islamic State (IS) katika ngome ya Raqqa nchini Syria kuoana na mpiganaji mmoja.

Mama yake Monique alisaidia kumrejesha nyumbani Uholanzi na si mtuhumiwa.

Aicha ni mmoja wa idadi ndogo ya wasichana na wanawake kutoka Ulaya ambao wamekwenda Syria na Iraq katika miezi ya karibuni.

Baadhi wanaaminika kusafiri kwenda hukokupata mafunzo ya kiitikadi, wakati wengine wanasemekana kuoana na wapiganaji, wakiwemo wanaopigana bega kwa bega na wapiganaji wa IS.

Mahakama nchini Uholanzi Ijumaa itasikiliza kesi hiyo bila wasikilizaji na itaamliwa Aicha anaweza kushikiliwa kwa muda gani.

Upande wa mashitaka unatarajiwa kumwomba jaji kuongeza muda wa kumshikilia Aicha wakati wakichunguza ushahidi.