Boko haram lawaua watu 95 Nigeria.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Boko haram lashambulia wauza samaki

Ripoti kutoka kazkazini mashariki mwa Nigeria zinasema kuwa wapiganaji wa Boko Haram wamefanya shambulizi jengine kubwa na kuwaua karibia wafanyibisahara hamsini wa kuuza samaki katika ufuo wa ziwa Chad.

Shambulizi hilo lilifanyika siku ya alhamisi kufuatia kuharibiwa kwa mtandao wa simu katika eneo hilo na kundi hilo,swala lililosababisha habari hizo kuwafikia raia kuchelewa.

Siku moja kabla,zaidi ya watu 40 waliuawa na wapiganaji hao katika shambulizi la mchana katika soko ndani ya jimbo la Borno.

Inadaiwa kuwa wafanyibiashara hao walikuwa wanaelekea Chad kununua samaki wakati wapiganaji hao walipovamia.

Walifunga barabara karibu na kijiji cha Doron Baga na kulingana na mkuu wa chama cha wauza samaki,wanamgambo hao waliwachinja wengi ya waathiriwa ,huku wengine wakifungwa na kuzamishwa katika ziwa hilo.

Haijabainika lipi lengo la mashambulizi hayo.Muungano wa wanajeshi kutoka mataifa hayo ikiwemo Nigeria ,Chad na Niger ulitarajiwa kupiga doria katika eneo hilo lakini vikosi hivyo vimeshindwa kuzuia mauaji hayo.