Njama ya polisi kumvua mwanamke nguo yatibuka

Image caption Baadhi ya wanawake walioandamana kupinga kitendo cha mwanamke kuvuliwa nguo kwa lazima nchini Kenya

Afisa mmoja wa polisi wa utawala nchini Kenya ni miongoni mwa wanaume waliokamatwa kwa kujaribu kumvua nguo mwanamke katika mtaa wa Komarock viungani mwa mji mkuu Nairobi.

Polisi walisema watu wanne walimsingira mwanamke huyo alipokuwa anaenda nyumbani kutoka kanisani akiwa ameandamana na rafiki yake.

Wanaume hao walijaribu kumvua nguo mmoja wa wanawake hao ila waliokolewa na wananchi waliokuwa wakielekea makwao.

Wanaume wawili waliokuwa wanawaokoa wanawake hao walijeruhiwa.

Kwa mujibu wa taarifa za mtandao wa Daily Nation, Kioo cha basi iliyokuwa barabarani pia kilivunjika katika purukushanio hilo.

Polisi waliofika katika eneo la tukio waligundua kuwa mmoja wa waliowashambulia wanawake hao alikuwa afisa wa polisi.

Tukio hilo limefanyika siku chache tu baada ya mamia ya wanawake kuandamana mjini Nairobi kulaani kitendo cha kumvua mwanamke mmoja mavazi yake yakisemekana kutokuwa na heshima.