Nigeria:Raia watakiwa kuwa waangalifu

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Rais wa Nigeria Goodluck Johnathan amewataka raia kuwa waangalifu kufuatia shambulizi la bomu katika msikiti mmoja nchini humo

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan amewataka watu wote nchini Nigeria kuwa waangalifu na kushirikiana na vikosi vya usalama vya nchi hiyo ili kujaribu kuzuia mashambulizi zaidi yanayotekelezwa na wanamgambo wa Boko Haram kaskazini mwa nchi.

Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulizi hilo lililotokea kwenye msikiti mmoja mkubwa ulio kwenye mji wa Kano ambapo watu kadhaa waliuawa.

Hata hivyo shambulizi hilo linaaminika kutekelezwa na Boko Haram ambalo kampeni yake dhidi ya serikali imesababisha vifo vya maelfu ya watu mwaka huu.

Polisi walitibua njama ya shambulizi jingine kwenye mji ulio kaskazini mwa Nigeria wa Maiduguri ambapo mabomu sita yaliharibiwa ndani ya msikiti mmoja na kwenye soko lililo karibu.