ICC yakataa ombi la muasi Lubanga

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mahakama ya ICC imetupilia mbali ombi la Lubanga kupunguziwa kifungo jela

Mahakama ya kimataifa ya ICC mjini Hague, imetupilia mbali ombi la rufaa lililowasilishwa na muasi wa zamani nchini DRC Thomas Lubanga dhidi ya hukumu aliyopewa kwa makosa ya kuwatumia watoto kama wanajeshi.

Viongozi wa mashtaka walisema wavulana wadogo wenye umri wa miaka 10 walitekwa nyara na kusajiliwa kama wanajeshi DRC katika vita hivyo vilivyoanza mwaka 1999.

Wasichana nao walitumiwa kama watumwa wa ngono.

Mnamo mwaka 2012, Lubanga alikuwa mtu wa kwanza kuhukumiwa na mahakama hio.

Aliwahi kuwa kiongozi wa kundi la wapiganaji la (UPC), ambalo lilikuwa la kabila la Hema ambalo lilihusika katika vita eneo la Ituri Mashariki mwa DRC.

Mahakama ilimpata na hatia kwa kuwatumia watoto kama wanajeshi na kuwatuma kwenda kumpigania. Alihukumiwa kifungo cha miaka 14.

Kundi la UPC, lilikuwa moja ya makundi sita ya wapiganaji waliopigana kudhibiti eneo lenye utajiri wa madini la Ituri hadi mwaka 2003.

Mgogoro ulianza kama mvutano wa kupigania mali asili, ingawa baadaye ilipanda daraja na kuwa vita vilivyohusisha jeshi la Uganda.

Kadhalika mgogoro huo uligeuka na kuwa vita kati ya jamii za Hema na Lendu ambapo takriban watu 50,000 waliachwa bila makao.