Tanzania: Uchuguzi kuendelea " Escrow"

Image caption Spika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda

Bunge la Tanzania mwishoni mwa wiki limehitimisha mkutano wake wa 17 ambao pamoja na mambo mengine lilijadili taarifa maalum ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, PAC kuhusu taarifa ya ukaguzi maalum kuhusiana na miamala iliyofanyika katika akaunti ya ESCROW ya TEGETA pamoja na umiliki wa Kampuni ya kufua umeme ya IPTL na kutoa maazimio juu ya sakata hilo.

Miongoni mwa maazimio manane ya Bunge ni kuchukuliwa kwa hatua za kisheria dhidi ya watu wote watakaobainika kuhusika na upotevu wa fedha hizo, kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 300 zilichotwa katika akaunti hiyo iliyokuwa iliyokuwa kwenye Benki Kuu ya Tanzania na ikimilikiwa kwa pamoja na IPTL na Shirika la Umeme Tanzania, TANESCO.

Image caption Bunge la Tanzania

Baadhi ya viongozi na maafisa wa serikali kama vile mawaziri, majaji, wabunge, wenyeviti wa kamati za Bunge, wakuu wa taasisi za umma, viongozi wa dini, mawakili wa kujitegemea na watu binafsi wanatuhumiwa kunufaika na mabilioni ya fedha kutoka akaunti ya Escrow na hivyo hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao kwa mujibu wa sheria za nchi.

Pia wabunge wametaka mikataba mibovu ya kuzalisha umeme kati ya TANESCO na makampuni binafsi ya kufua umeme iwasilishwe bungeni au kamati zake kwa lengo la kutekeleza vyema wajibu wake wa kuisimamia na kuishauri serikali.

Kwa miaka mingi TANESCO imekuwa ikilalamika kulipa gharama kubwa za umeme na kusababisha kupanda kwa gharama za matumizi ya nishati hiyo nchini Tanzania.