AFCON 2015:Makundi ya timu 16 yatajwa

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, AFCON

Upangaji wa makundi ya timu kumi na sita zilizofuzu kucheza fainali za mashindano ya 30 ya kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mwaka 2015 yamefanyika katika mji mkuu wa Equatorial Guinea, Malabo.

Mashindano hayo yataanza Januari 17, 2015.

Upangaji wa makundi ulirudishwa wiki moja nyuma ili kuiwezesha Equatorial Guinea, kujiandaa baada ya kuchukua nafasi ya Morocco, iliyokuwa iandae mashindano hayo, lakini ilishindwa kufanya hivyo baada ya kutaka mashindano hayo yasogezwe mbele kuhofia ugonjwa wa Ebola ambao umeyakumba baadhi ya mataifa ya Afrika Magharibi, ambako zinatoka timu nyingi zinazoshiriki michuano hiyo.

Mabingwa watetezi Nigeria ni moja ya timu kubwa zilizoshindwa kufuzu kucheza fainali za mwakani, pamoja na Misri na Angola ambazo zote kwa mshangao hazitaweza kushiriki.

Haya hapa makundi manne ya AFCON 2015:

Kundi A Equatorial Guinea, Burkina Faso, Gabon, Congo

Kundi B Zambia, Tunisia, Cape Verde, DR Congo

Kundi C Ghana, Algeria, South Africa, Senegal

Kundi D Ivory Coast, Mali, Cameroon, Guinea

Wenyeji Equatorial Guinea na Congo zitacheza mechi ya ufunguzi wa michuano hiyo. Kundi D ndilo linaloonekana kuwa gumu zaidi kutokana na timu zilizopangwa kundi hilo.