Ebola yauwa daktari mwengine S-Leone

Dakta Sheik Umar Khan  aliyefariki mwezi Julai Haki miliki ya picha BBC World Service

Wakuu wa Sierra Leone wanasema daktari mwengine amefariki kutokana na Ebola - ni daktari wa 10 kufa na ugonjwa huo.

Aiah Solomon Konoyima alifariki Jumamosi kwenye kituo cha matibabu karibu na mji mkuu, Freetown, siku moja tu baada ya wenzake wawili kufa na ugonjwa huo huo.

Mwezi wa Julai daktari maarufu kabisa kutibu wagonjwa wa Ebola nchini Sierra Leone, Sheik Umar Khan, piya mwisho aliuliwa na virusi vya Ebola.

Vifo 1,600 vya Ebola vimesajiliwa nchini humo.

Sierra Leone imekuwa ikijaribu kukarabati huduma za afya baada ya vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe katika miaka ya 1990s.

Na daktari kutoka Cuba ambaye alipona Ebola, ameahidi kuwa atarudi Sierra Leone kumaliza kupambana na ugonjwa huo nchini humo.

Dakta Felix Baez, ambaye alipata Ebola nchini Sierra Leone, alisema hayo aliporudi Havana baada ya kujaribiwa matibabu aina mpya nchini Uswiswi ambayo yalimponesha.

Dakta Baez alikuwa kati ya madkatari na wauguzi wa kwanza 250 walioambukizwa Ebola Afrika magharibi.

Cuba ndio nchi iliyotuma huko wafanyakazi wa utabibu wengi kabisa kwenda kupambana na Ebola.

Mchango huo wa Cuba umesifiwa kimataifa hata na Marekani, adui yake wa kisiasa.