Rais Mugabe amfuta kazi makamu wake

Haki miliki ya picha
Image caption Joyce Mujuru anasema serikali inamuharibia sifa wala haina ushahidi wowote dhidi yake

Taarifa kutoka nchini Zimbabwe zinasema kuwa Rais Robert Mugabe amemfuta kazi makamu wake Joice Mujuru, kufuatia ushindani wa uongozi katika chama tawala cha ZANU-PF.

Awali Bi Joyce Mujuru, alikanusha madai kuwa yeye ni mfisadi na alihusika na njama ya kutaka kumuua rais Robert Mugabe.

Bi Mujuru alilaaniwa na Rais Mugabe wiki iliyopita na kuondolewa kutoka wadhifa wake wa makamu wa rais wa chama tawala cha ZANU-PF wakati wa kongamano la chama hicho mjini Harare.

Amesema ameendelea kupokea vitisho na kuwa shirika la habari la serikali limeendelea kuchapisha habari za uongo za zisizo na msingi dhidi yake.

Ilikuwa wiki nzima ya tuhuma dhidi ya Bi Mujuru kutoka kwa vyombo vya habari vya serikali kwa ushirikiano na mkewe Mugabe, Grace Mugabe, ambaye kwa sasa ameteuliwa kama afisaa mkuu wa chama cha ZANU-PF.

Wengi walimuona Mujuru mwenye umri wa miaka 59, kama mrithi wa Mugabe.

Katika hatua yake ya kwanza kujibu tuhuma hizo tangu kuondolewa katika chama, Mujuru alisema amekuwa akitishiwa sana na watu asio wajua.

Aliongeza kuwa vyombo vya habari nchini humo vimeendelea kumchafulia jina lake kwa kuchapisha porojo na taarifa za uongo, dhidi yake.

Alisema hakuna hjata tone moja la ushahidi limetolewa dhidi yake kuthibitisha madai anayasingiziwa na kutajwa kuwa msaliti mkubwa.

Madai kuwa alipanga njama ya kumuondoa mamlakani Mugabe, ni ya kipuzi sana.

Rais Mugabe, mwnye umri wa miaka 90, amekua mamlakani tangu Zimbabwe kujipatia uhuru mwaka 1980.

Bi Mujuru alipambana bega kwa bega na Mugabe mapema miaka ya 1970, dhidi ya utawala wa kibaguzi na kwa wengi alionekana kama mrithi mtarajiwa wa Mugabe.