Mugabe amteua makamu mpya wa Rais

Image caption Emmerson Mnangagwa ndiye makamu mpya wa Rais baada ya kuteuliwa na Rais Mugabe

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe amemteua makamu mpya wa Rais Emmerson Mnangagwa dalili kwamba huyo ndiye Mugabe anampendekeza kumrithi.

Bwana Mnangagwa anachukua wadhifa huo kutoka kwa Bi Joyce Mujuru ambaye Mugabe alimfuta kazi baada ya kumtuhumu kupanga njama ya kumuua.

Kwa jina la mzaha Mnangagwa anajulikana kama 'Mamba' mmoja wa watu wenye msimamo mkali wa chama.

Mugabe,mwenye umri wa miaka 90, alifanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri mnamo siku ya Jumanne huku akiendelea kung'ang'ania mamlaka.

Image caption Mkewe Mugabe, Grace ni kiongozi wa tawi la wanawake wa chama hicho

Alichaguliwa kwa mara nyingine kama kiongozi wa chama tawala Zanu-PF katika kongamano lake mwishoni mwa wiki wakati mkewe mwenye umri wa miaka 49, Grace akiteuliwa kuongza tawi la wanawake wanachama wa chama hicho.

Katika kauli yake ya kwanza tangu kupandishwa cheo, Bwana Mnangagwa alionekana kuunga mkono mabadiliko yaliyofanywa katika chama hicho.

Bi Mujuru mwenye umri wa miaka 59, alionekana kama tisho kubwa kwa bwana Mnangagwa katika ushindani wa uongozi wa chama hicho wakati Mugabe atastaafu au kufariki.

Vyombo vya habari vya serikali kwa ushirikiano na Bi Grace Mugabe vimekuwa vikiendesha kampeini ya kumchafulia jina Bi Mugabe.

Hata hiuvyo amekanusha madai hayo akisema hakuna hata ushahidi mmoja umetolewa dhidi yake kuthibitisha madai hayo kuwa alipanga njama ya kumuua Mugabe ili amrithi kama kiongozi wa chama.