Jeshi latahadharishwa kuhusu mitandao

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Maafisa wa jeshi waelezwa kuwa makini kabla ya kutumia mitandao ya kijamii

Jeshi la nchini India limewataadharisha maafisa wake kuwa makini na vitendo vya kupokea ujumbe au kutuma tena ujumbe waliotumiwa na watu wengine bila kuchunguza ukweli wake.

Jeshi pia limewataka maafisa wanaotumikia jeshi na waliostaafu wanaotumia mitandao ya kijamii kuwa makini wanaposukuma ujumbe ambao unaweza kuathiri sifa ya Jeshi.

Imeripotiwa kuwa siku za hivi karibuni, kumekuwepo na jaribio la kuharibu sifa ya Jeshi kwa makusudi kwa kuweka taarifa zisizothibitika ukweli wake.

Hatua hii imekuja baada ya Luteni Jenerali mmoja kaskazini mwa India DS Hooda kukubali kuwa lilikuwa ''kosa'' lililofanywa na maafisa wake kuhusika na mauaji ya raia wawili mwezi uliopita.

Tukio hilo lilisababisha kuwepo na kauli nyingi za kukemea na kushutumu lakini Hooda aliwaambia maafisa wake kutokujiingiza kwenye malumbano na kauli zinazotolewa navyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Baada ya matukio ya kigaidi ya hivi karibuni kumekuwepo na ujumbe mwingi uliotembea ukishambulia utawala wa Jeshi nchini India, baadhi ya ujumbe pia unadaiwa kuandikwa na maafisa wa chini wa Jeshi.