Akiri kuwaua watu 42 nchini Brazil

Haki miliki ya picha AFP PHOTO POLICIA CIVIL
Image caption Sailson das Gracas amekiri kufanya mauaji hayo kwa sababu anasema alipenda kufanya hivyo

Polisi nchini Brazil wamemkamata mwanaume aliyekiri kuwaua watu 42 katika kipindi cha miaka kumi mjini Rio de Janeiro.

Polisi wanasema walimkamata Sailson Jose das Gracas mnamo siku ya Jumatano, baada ya kumdunga kisu mwanamke ambaye alifariki muda mfupi baadaye.

Alikiri kuwaua wanawake wengine 37 , wanaume watatu na mtoto mdogo wa miaka 2.

Polisi wanasema wanawasaka waathiriwa na kusema wameweza kuwapata watu wanne.

Katika mahojiano na vyombo vya habari, polisi walisema kua mwanamume huyo kawaida alikuwa anaondoka kwake na kuwawatufuta waathiriwa lengo lake likiwa ni kuua 'kwa raha zake.'

Aliambia polisi kuwa wakati atakapoondoka gerezani hatasita kuua tena.

Alisema kuwa alipendelea kuwaua wanawake wazungu ambao aliwanyonga.

Wanaume watatu ambao aliwaua, alifanya hivyo alipokodiwa kama mamluki.

Das Gracas alisema: " Ningesubiri kupata fursa tu kisha ningeingia ndani ya nyumba na kutekeleza mauaji,'' akiongeza kwamba angewachunguza waathiriwa wake kwa muda kabla ya kuwaua.

Wataalamu wanasema Das Gracas anaonekana kuwa mgonjwa wa kiakili ambaye alipenda sana kuonekana kwneye vyombo vya habari, na kuonya kuwa polisi wawe waangalifu sana kuhusu chochote anachosema.