Mahujaji milioni 17 wakusanyika Karbala

Waumini wakielekea Karbala Haki miliki ya picha bbc

Mamilioni ya mahujaji wa Kishia wamemiminika katika mji wa Karbala, Iraq, kwa ibada ya kila mwaka ya Arbaeen ingawa kuna tishio la mashambulio ya wapiganaji wa madhehebu ya Sunni wa Islamic State.

Wakuu wa Iraq wanasema mahujaji zaidi ya milioni 17 wamekusanyika Karbala kuhudhuria Arbaeen.

Picha zilizopigwa kutoka angani zinaonesha barabara zinazoelekea Karbala kama mito ya watu waliovaa nguo nyeusi, hadi upeo wa macho.

Na kuna wasiwasi kuwa mji wa Karbala hautaweza kuwapatia malazi waumini wote.

Ulinzi mkubwa umewekwa kuzuwia mashambulio ya wapiganaji wa Islamic State.

Arbaeen ni siku ya mwisho ya maombolezi baada ya kifo cha Imam Hussain cha karne ya 7 katika Vita vya Karbala - tukio muhimu ambapo Wasunni waligawanyika na Washia.