EU yakemea kukamatwa Wanahabari Uturuki

Haki miliki ya picha AP
Image caption Wafanyakazi wa kampuni ya Gazeti la zaman walipiga kambi nje ya mahakama jijini Istambul

Maafisa wakuu katika Umoja wa Ulaya wamepinga kukamatwa kwa wawakilishi wa vyombo vya habari nchini Uturuki.

Waziri wa mambo ya nje, Federica Mogherini na kamishina anayeongoza mazungumzo makuu katika EU amesema kwamba kukamatwa kwao ni "kinyume na maadili ya Ulaya".

Watu 24 walikamatwa baada ya polisi kuvamia ofisi za gazeti kuu na kituo cha televisheni kwa kusemekana kuwa uhusiano wa karibu na vyama vya upinzani.

Wale waliopo kizuizini wanatuhumiwa kwa kujaribu kupora udhibiti wa serikali.

Gazeti la Zaman na stesheni ya Samanyolu TV zote zina uhusiano na mhubiri wa Kiislamu, na kiongozi wa kiroho wa Hizmet, Fethullah Gulen ambaye anamakao Marekani.

Mshirika wa zamani wa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, Bw. Gulen - ambaye anaishi uhamishoni – anatuhumiwa kuongoza serikali sambamba ndani ya Uturuki.

Katika kauli ya pamoja, Bi Mogherini na Kamishna wa EU Johannes Hahn Walisema hatua yoyote kuelekea uanachama wa EU unategemea "heshima kamili kwa ajili ya utawala wa sheria na haki za msingi".

Uvamizi na kukamatwa kwa waandishi "haziendani na uhuru wa vyombo vya habari, ambayo ni kanuni ya msingi ya demokrasia," wote walisema katika kauli ya pamoja.

Uvamizi huo umetokea siku kadhaa baada ya Bw. Erdogan kuahidi kampeni mpya dhidi ya wafuasi wa Gulen.