Wapenzi wa jinsia moja hatarini Urusi

Haki miliki ya picha AP
Image caption Polisi wamkamata mwanaharakati wa mapenzi ya jinsia moja nchini Urusi

Ripoti mpya iliyotolewa na shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, imenasema kuwa visa vya wapenzi wa jinsia moja kushambuliwa vinaendelea kuongezeka hasa tangu serikali kupiga marufuku propaganda zozote kuhusu mapenzi ya jinsia moja mwaka jana.

Taarifa hio, ilitaja sheria ya serikali kama kibali cha kuwadhuru watu wengine likisema inaashiria kuwa watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja ni wananchi wa kiwango cha chini.

Wanaoiunga mkono sheria hiyo wanasemekana kuwa wahafidhina na wanataka maadili au utamaduni wa Urusi kusalia ulivyo.

Maisha hayajawahi kuwa rahisi kwa wapenzi wa jinsia moja nchini Urusi.

Lakini mashirika yanayotetea haki zao yanasema maisha yamekuwa magumu zaidi tangu sheria hio kupitishwa.

Human Rights watch linasema kuwa wanaharakati wamekuwa wakiripoti ongezeko la wapenzi wa jinsia moja kuhangaishwa na kuteswa na hata kushambuliwa

Wanasema yote hayo yanawakumba kwa sababu ya kupitishwa kwa sheria hio mwaka jana ambao serikali imeharamisha mfumo wa maisha usio wa kitamaduni.

Wakosoaji wanasema sheria hio inaonyesha kwamba wapenzi wa jinsia moja ni hatari na hawafai kwa jamii.

Shirika moja linasema zaidi ya watu 300 walishambuliwa mwaka jana katika vita dhidi ya mapenzi wa jinsia moja.

Wanaoiunga mkono sheria hio,wanasema mizizi ya kikristo ya urusi inapaswa kuheshimiwa na pia mapenzi ya jinsia moja ni mfumo potovu wa maisha wa kimagharibi.