Sigara ya bangi yaanza kuuzwa Uingereza

Image caption Sigara ya kielektroniki iliyo na bangi ndani yake imeanza kuuzwa nchini Uingereza.

Wakati sigara ya kwanza ya bangi ya kieletcroniki ilipozinduliwa mnamo mwezi juni ilikuwa ikipatikana ughaibuni pekee.

lakini sasa ,kampuni moja imechukua hatua zaidi na kuanza kuuza bidhaa hiyo katika maeneo ya Uingereza.

KanaVape kama kinavyojulikana ni kifaa ambacho kina fanana na sigara za kielektroniki lakini chenye Bangi, kitauzwa mitandaoni kuanzia alhamisi ijayo,kulingana na mtandao wa Metro nchini Uingereza.

Watengezaji wa bidhaa hiyo nchini Uingereza Atonin Cohen na Sebastien Beguerie wanadai kwamba bidhaa hiyo ni halali kwa kuwa haina kemikali za bangi zinazoathiri akili.

Bidhaa hiyo inatumia asilimia tano ya bangi,ikimaanisha kuwa inampa mteja hisia za utulivu kama bangi lakini haina athari zozote mbaya.

Bidhaa hiyo ya E-joint inamaanisha kuwa mtumiaji anaweza kuvuta mvuke wa bangi bila kupata harufu ya kawaida ya moshi wake.

Mashirika ya madawa hatahivyo yameipinga bidhaa hiyo kama kitu kilichotengezwa ili kuvutia hisia,lakini yakasema kuwa kuna uwezekano mkubwa kwamba bidhaa hiyo itakuwa halali chini ya sheria ya Uingereza kwa kuwa haina kemikali yenye madhara.