230 wauawa na IS Syria

Image caption Islamic State

Miili ya Watu zaidi ya 230 wanaoelezwa kuawa na Wanamgambo wa Islamic State imepatikana katika kaburi la pamoja mashariki mwa Syria, Wanaharakati wameeleza.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais wa Syria Bashaar Al Assad

Shirika la uangalizi wa haki za binaadam la Syria limesema Watu hao wanakisiwa kuwa jamii ya kabila moja lililokuwa likipambana na kundi la Jihad jimbo la Deir al-Zour.

Kaburi la pamoja liligunduliwa baada ya Watu wa jamii ya kabila la Sheitat kuruhusiwa na Viongozi wa Wanamgambo wa IS kurejea nyumbani.

Mwezi uliopita , Umoja wa Mataifa ulisema umepokea ripoti kuhusu mauaji mjini humo mwezi Agosti.

Wachunguzi wanasema kuwa inaonyesha kuwa mauaji hayo yalitekelezwa na wanamgambo wa Islamic State katika harakati ya kudhibiti rasilimali ya mafuta karibu na Mji wa Mohassan.

Mmoja kati ya manusura amesema aliona vichwa vingi vikiwa vimening'inizwa kwenye kuta, lakini yeye alifanikiwa kutoroka na familia yake.

Mauaji yanaripotiwa kutokea baada ya mazungumzo kati ya pande hizo mbili kuvunjika huku jamii ya kabila la Sheitat ikikataa kutekeleza yale waliyokubaliana na IS.