Indonesia wakumbuka Tsunami

Haki miliki ya picha REUTERS
Image caption Wanawake eneo la Aceh wakifanya sala ya kukumbuka maafa makubwa yaliyosababishwa na tsunami miaka kumi iliyopita nchini Indonesia

Wananchi wa Indonesia wameanza kuadhimisha mwaka wa kumi tangu kutokea kwa tetemeko la ardhi lililosababisha mawimbi makubwa katika bahari ya Hindi, tsunami na kusababisha vifo vya watu zaidi ya watu laki mbili na elfu ishirini katika eneo kubwa.

Umati wa watu umekusanyika karibu na jengo la makumbusho la tsunami katika eneo la Banda Aceh katika kisiwa cha Sumatra.

Mji huo ulisambaratishwa kabisa na tetemeko kubwa la ardhi na mawimbi ya tsunami. Makamu wa Rais wa Indonesia(Jusuf Kalla) anaongoza maadhimisho hayo na atawashukuru wafanyakazi wa kujitolea katika eneo hilo na duniani kote kwa kulisaidia eneo la Aceh kurejea katika hali ya kawaida baada ya mkasa huo.