Washtakiwa Marekani kwa uhaini Gambia

Haki miliki ya picha
Image caption Rais wa Gambia, aliyetaka kupinduliwa.

Marekani imewafungulia mashitaka watu wawili kwa kuhusika na jaribio la kutaka kuiangusha serikali ya Gambia wiki iliyopita.

Wizara ya Sheria ya Marekani imesema watuhuhumiwa hao wawili, Cherno Njie na Papa Faal, wameshitakiwa kwa kula njama dhidi ya taifa rafiki wa Marekani na kula njama ya kumiliki silaha ili kuendeleza uhalifu.

Washitakiwa wote ni wenye asili ya Gambia.

Taarifa kutoka Gambia inasema majeshi ya usalama yanaendelea kuwakamata ndugu wa watuhumiwa wanaotajwa kuhusika katika jaribio lililoshindwa la kuiangusha serikali ya Gambia, Jumanne ya wiki iliyopita katika makazi ya rais.

Wizara ya Sheria ya Marekani imesema, kwa mujibu wa nyaraka zilizowasilishwa mahakamani, watuhumiwa wote wawili walisafiri kutoka Marekani kwenda Gambia kwa lengo la kuiangusha serikali ya nchi hiyo.

Wizara hiyo imesema mmoja wa watu hao, Cherno Njie mwenye umri wa miaka 57, alikuwa kiongozi wa njama hizo na angeteuliwa kuwa kiongozi wa mpito wa Gambia iwapo jaribio la kuiangusha serikali lingefanikiwa.

Mtuhumiwa mwingine ni Papa Faal, mwenye umri wa 46 ambaye amedaiwa kuhusika katika jaribio hilo. Pia imeelezwa kuwa silaha zikiwemo bunduki za rashasha, na vifaa vingine vya kijeshi vilisafirishwa mwaka jana kwenda Gambia kutumika katika jaribio la kuangusha serikali.

Watu hao wawili walikamatwa baada ya kurejea Marekani wiki iliyopita.

Njie mkazi wa Austin, Texas atafikishwa katika mahakama ya Baltimore, Maryland. Faal atafikishwa katika mahakama ya mji wa Minneapolis, Minnesota.

Watuhumiwa wote wawili wameshitakiwa kwa kukiuka sheria ya kutojishirikisha na masula ya nchi nyingine kwa kula njama ya kuiangusha serikali ya nchi rafiki na Marekani na kula njama ya kumiliki silaha katika kuendeleza uhalifu na ghasia nchini Gambia. Desemba 30, 2014, kulifanyika jaribio ambalo halikufanikiwa la kuiangusha serikali ya Gambia. Gambia ni nchi iliyoko Afrika magharibi ikipakana na nchi ya Senegal na bahari ya Atlantic.

Njie na Faal ni raia wa Marekani wenye asili ya Gambia.