Yanga yang'ara Kombe la Mapinduzi

Haki miliki ya picha Yanga
Image caption Timu ya Yanga ya Dar es Salaam

Michuano ya kuwania Kombe la Mapinduzi Zanzibar, linalozishirikisha timu saba za Zanzibar, nne za Tanzania Bara na KCCA kutoka Uganda imezidi kupamba moto ikiwa katika hatua ya kukamilisha michezo ya makundi.

Timu ya Yanga ya Tanzania Bara imezidi kutoa vipigo kwa timu za kundi lake baada ya kuzicharaza timu za Taifa Jang'ombe na Polisi zote za Zanzibar magoli 4-0 kila moja na hivyo kujikusanyia mabao nane na pointi sita ikiwa haijaruhusu nyavu zake kutikiswa na timu pinzani na hivyo kuongoza kundi A lenye timu za Taifa Jang'ombe, Polisi Zanzibar na Shaba pia ya Zanzibar.

Kwa matokeo hayo imefuzu kucheza hatua ya robo fainali.

Wapinzani wao wakubwa pia kutoka Bara, Simba imekuwa na mwendo wa kusuasua ambapo katika mchezo wake wa kwanza katika kundi C ilicharazwa na Mtibwa Sugar bao 1-0 kabla ya kuzinduka na kujipatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar. Katika kundi hilo Simba ina timu za Mtibwa Sugar ya Tanzania Bara, Mafunzo ya Zanzibar na JKU Zanzibar.

Kundi B lina timu za KCCA ya Uganda, Azam ya Tanzania Bara, KMKM na Mtende zote za Zanzibar.

Januari saba michuano hiyo itaingia hatua ya robo fainali kwa timu sita kutoka makundi yote matatu yenye jumla ya timu 12.