Steven Gerrard aibeba Liverpool FA

Image caption Steven Gerrard, nahodha wa timu ya Liverpool akishangilia bao na wachezaji wenzake katika moja ya mechi alizoichezea timu hiyo

Steven Gerrard ameonyesha ubora na uongozi na Liverpool itamkosa mchezaji wa aina hii wakati atakapohama Anfield.

Ni Gerrard aliyewainua mara mbili vitini mashabiki wa Liverpool ilipoizamisha AFC Wimbledon mabao 2-1 katika michezo inayoendelea ya Kombe la FA.

Gerrard, akicheza mchezo wake wa kwanza tangu atangaze kuihama Liverpool katika msimu ujao na kwenda kukipiga Marekani, alionyesha pengo atakaloliacha atakapoihama timu yake aliyokulia na kupata mafanikio makubwa.

Nahodha huyo wa Liverpool ambaye atasherehekea miaka 35 katika siku ya mwisho ya Kombe la FA, tarehe 30 mwezi Mei aliiongoza timu hiyo kupata mafanikio na amefanya hivyo mara nyingi wakati timu ilipojikuta katika matatizo.

Gerrard alianza kuichezea Liverpool mwaka 1998. Gerrard amefunga magoli 182 katika michezo 696 aliyoichezea timu ya Liverpool.

Na katika mchezo mwingine Tottenham walitoka sare na Burnley kwa kufungana goli 1-1. Burnley ndio waliokuwa wenyeji wa mchezo huo.