Wachora vibonzo stadi wauawa Ufaransa

Image caption Shambulio katika kituo kimoja cha magazeti nchini Ufaranza

Wanaume waliokuwa wamejifunika nyuso wamewaua takriban watu 12 katika ofisi za gazeti moja la vibonzo la Charlie Hebdo mjini Paris Ufaransa.

Watu wengine saba wameripotiwa kujeruhiwa vibaya.

Gazeti hilo lililo mjini Paris limekuwa likilengwa na wanamgambo wa kiislamu siku za nyuma kiasi cha kutoa vitisho vya mauaji kwa mhariri mkuu wa jarida hilo.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Jarida la Charlie Hebdo huangazia maswala mbali mbali kw akutumia vibonzo

Tukio hilo lilitokea mapema asubuhi wakati watu waliokuwa na silaha walipoingia katika ofisi za gazeti hilo na kuanza kufyatua risasi na kisha wakatoroka kwa gari.

Polisi wanafanya msako mkubwa kuwatafuta washambuliaji huku mji wa Paris ukiwa chini ya tahadhari kubwa.

Rais wa ufaransa Francois Hollande amelaani shambulizi hilo akisema kuwa nchi hiyo imepatwa na mshangao mkubwa.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Inaarifiwa watu watano walijeruhiwa katika uvamizi huo

Washambuliziji watatu waliokuwa wamefunika nyuso zao, walifyatuliana risasi na polisi nje ya jengo la ofisi za shirika hilo la habari kabla ya kutoroka.

Inaarifiwa washambulizi walisikika kwa sauti ya juu wakisema ''tumelipiza kisasi kw aniaba ya Mtume Muhammad.'

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Rais Francois Hollande anasema hana shaka kwamba shambulizi hilo lilikuwa la kigaidi

Rais Francois Hollande alisema hapana shaka kwamba shambulizi hilo ni la kigaidi

Waandishi wanne wa jarida hilo la vibonzo, akiwemo mhariri mkuu Stephane Charbonnier walikuwa miongoni mwa waliouawa pamoja na maafisa wengine wawili.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Athari za risasi lililogonga dirisha la ofisi za jarida hilo

Bwana Charbonnier, mwenye umri wa miaka 47, aliwahi kupokea vitisho vya kuuawa na alikuwa analindwa vikali na polisi.

Vyombo vya habari vimewataja wachoraji wengine watatu waliouawa wakiwemo, Cabu, Tignous na Wolinski. Duru zinasema shambulizi hilo lilifanyika wakati wa mkutano wa kila mwezi wa uhariri wa jarida hilo.