Shell yakubali kulipa fidia Nigeria

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Kampuni ya Shell nchini Nigeria

Kampuni kubwa ya mafuta ya Shell imekubali kulipa dola milioni 80 kama fidia.

Kampuni hiyo ya Uholanzi imewapa fidia wakazi wa jamii ya Bodo katika eneo la Niger Delta walioathiriwa na uvujaji wa mafuta.

Mawakili wa wavuvi 15,600 wa Nigeria wamesema wateja wao watapokea dola za Kimarekani 3,300 kila mmoja kutokana na hasara iliyosababishwa na uvujaji wa mafuta hayo.

"Kiasi kilichobaki cha dola milioni 30 zitatumika kwa ajili ya shughuli za jamii ya Bodo ambayo iliathirika vibaya kutokana na matukio mawili ya kuvuja mafuta mwaka 2008 na 2009".

Mawakili hao wamesema mafuta hayo yaliharibu maelfu ya hekta za mikoko kusini mwa Nigeria.

Fidia hiyo imesemekana kuwa kuwa kubwa kuwahi kuliko zote zilizowahi kulipwa nchini Nigeria, na hivyo kumaliza mvutano wa kisheria uliodumu kwa miaka mitatu. Wanaharakati wanasema kampuni ya Shell ililazimika kukiri kosa hilo mapema zaidi.

Matukio yote mawili ya kuvuja kwa mafuta yametokea katika bomba hilo hilo la Trans Niger Pipeline, linaloendeshwa na kampuni ya Shell, ambalo linachukua mafuta kutoka visima vyake(Shell) kwenda kituo cha mwisho cha kusafirisha mafuta hayo nje kilichopo pwani ya Bonny. Bomba hilo linasafirisha mapipa 180,000 ya mafuta kwa siku.