Je,shahidi wa ICC aliyeuawa ni nani?

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mahakama ya ICC

Hadi kutoweka kwake katika hali ya kutatanisha na baadaye kifo chake cha kushangaza ambacho kimevutia hisia tofauti ulimwenguni,jina Meshack Yebei halikuwa likijulikana zaidi ya kijiji chake cha Sugoi Magharibi mwa Kenya.

Lakini sasa mtu huyo anayeelezewa kuwa shahidi muhimu aliyetarajiwa kutoa ushihidi katika mahakama ya uhalifu wa kivita ICC katika kesi dhidi ya naibu wa rais William Ruto ni swala la kushangaza vilevile.

Marehemu Yebei mwenye umri wa miaka 34 alitoweka tarehe 28 mwezi Disemba na mwili wake uliokuwa na majereha kupatikana ukiolea katika mto mmoja karibu na mji wa Eldoret.

Familia na wanaharakati wa haki za kibinaadamu wanasema alitekwa nyara na kuuawa kinyama kwa kuhusishwa na kesi ya ICC nchini Kenya.

Wale waliokuwa karibu naye walimuelezea Meshack Yebei kama mwanasiasa mwenye utata ambaye haikuwa rahisi kumshawishi licha ya uamuzi huo kuwa muhimu vipi.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Ramani inayoonyesha maeneo yaliokumbwa na vita wakati wa uchaguzi wa mwaka 2007 nchini kenya

Alishiriki katika maswala mengi ya kijamii katika kaunti ya Uasin Gishu.

Alikuwa mmiliki wa taasisi ya kompyuta katika mji wa Eldoret.

Mnamo mwaka 2002,Meshack Yebei hakufaulu kushinda kiti cha udiwani cha Tapsagoi katika kaunti ya Uasin Gishu.

Alikuwa mgombea kupitia tiketi ya chama cha NARC,muungano wa vyama vya upinzani ambavyo viliunda muungano ambao ulikiondoa chama tawala cha KANU katika utawala.

Wakati wa uchaguzi mkuu wa 2007 nchini Kenya,Meshack Yebei alikuwa mshirikishi wa chama cha Mwai Kibaki PNU katika wilaya ya Uasin Gishu.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Luois Moreno Ocampo ,aliyekuwa kiongozi wa mashtaka kayika mahakama ya ICC

Jukumu lake lilikuwa kuandaa mikutano ya wagombea wa udiwani na ubunge wa chama cha PNU katika wilaya hiyo.

Wilaya ya Uasin Gishu ndio iliokuwa kitovu cha mapigano ya kikabila kufuatia uchaguzi wa mwaka 2007.

Kisa kibaya zaidi kuwahi kutokea katika eneo hilo ni kile cha kuchomwa kwa kanisa la kiambaa KAG karibu na mji wa wilaya ya Eldoret ambapo zaidi ya watu 40 waliuawa.

Kisa hicho kilihusishwa pakubwa katika kujenga kesi dhidi ya William Ruto.

Lakini wakati huo Bwana Ruto alikuwa mbunge wa muungano wa upinzani kwa jina ODM.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption William Ruto akiwa na mwandishi joshua sanga katika mkutano na vyombo vya habari

Ilipofikia uchaguzi wa mwaka 2013,Meshack Yebei aligombea tena.Aliwania kiti cha udiwani cha Tapsagoi kama mgombea huru.

Tapsagoi ni nyumbani kwa William Ruto.

Yebei alikuwa wa tatu katika uchaguzi ambao mgombea wa chama cha Ruto cha URP aliibuka mshindi.

Hadi kifo chake wiki iliopita ,nduguze wanasema Meshack alikuwa mwanasiasa shupavu lakini alijihusisha sana na biashara yake ya kununua na kuuza mbegu kama vile mahindi ili kupata pato la kuishi.