Hali tete kaskazini Mashariki-Nigeria .

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Askari wakiranda mjini Baga.

Maofisa wa serikali nchini Nigeria wamesema kwamba wameshindwa kukadiria kiwango cha vurugu eneo la Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo kwenye mji wa Baga,vurugu ambazo zimesababisha maelfu ya vifo vya raia.

Mji huo una kambi ya kijeshi ambao kwasasa uko chini ya udhibiti wa wanamgambo wa kundi la kigaidi maarufu kama Boko Haram.

Katika mji huo wa Baga maafisa hao wanakiri ya kwamba ni vigumu kupata idadi kamili ya vifo kwenye mji huo na vijiji vinavyo zunguuka mji huo,kwasasa mji huo unadhibitiwa na Boko Haram, hivyo si salama kwa yeyote kuingia na kuhesabu vifo akiwa peke yake wakati kuna huduma ya maziko pia inahitajika.

Seneta wa mji huo,Maina Maaji Lawan, anasema kwamba anaamini maelfu ya raia wake wameuwana wengine wakiyakimbia makaazi yao kwenda kutafuta makazi salama.

Seneta huyo anaendelea kueleza aliyoyashuhudia mjini Baga kwamba askari wa kundi hilo la Boko Haram,wameharibu vyakula na dawa na kuyachoma majengo ya mji wa Baga.

Seneta huyo ameiambia BBC kwamba maelfu ya raia wamevuka mpaka na kuingia nchini Chad,na huko wamejikuta wako njia panda kwa kukosa huduma muhimu za kibinadamu.

Hali mbaya Zaidi inashuhudiwa upande wa Kaskazini Mashariki mwa Nigeria kwani hali ya utu ina zidi kudidimia.katika hali ya kustaajabisha rais wa Nigeria Goodluck Jonathan ameyatazama mauaji ya mjini Paris na kutuma salamu zake za rambi rambi na kuyaeleza kama ya kishetani huku akishindwa kunyanyua mdomo kwa matokeo ya mashambulizi ya kikundi cha askari wa Boko Haram.Nao wanasiasa wakubwa nchini humo mawazo yao yote yameelekezwa katika uchaguzi utakao fanyika mwezi ujao.