Ebola:Kenya kuwatuma maafisa 170 wa afya

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wafanyikazi wa afya katika mataifa yanayokumbwa na ugonjwa wa Ebola

Wafanyikazi 170 wa afya wanatarajiwa kuondoka nchini Kenya na kuelekea nchini Sierra Leone na Liberia siku ya ijumaa kama ujumbe wa Umoja wa Afrika wa kudhibiti Ebola Afrika magharibi.

Maafisa hao waliojitolea kutoka kaunti 47 nchini Kenya watakuwa Afrika Mgharibi kwa miezi sita.

Wamefunzwa hali ya kujikinga na kusimamia ugonjwa huo na wizara ya afya,shirika la afya duniani pamoja na washirika wengine.

Maafisa hao wanaoshirikisha madaktari ,wauguzi na maafisa wengine wa afya wanatarajiwa kutoa huduma mbalimbali kama vile kuwahudumia wagonjwa na wafanyikazi wa maaabara kulingana na ujuzi wao na mahitaji yaliopo.

Hatua ya kuwapeleka katika mataifa hayo inajiri wakati ambapo kuna uhaba wa maafisa 5,000 wa afya wanaohitajika ili kuweza kukabiliana na ugonjwa huo kulingana na banki ya dunia.