Zaidi ya milioni waandamana Ufaransa

Mwenyejei Rais Hollande na wageni  wake wakishiriki kwenye maandamano mjini Paris Haki miliki ya picha bbc

Watu zaidi ya milioni wameandamana taratibu mjini Paris, wengi wakiwa wamebeba mabiramu na kupepea bendera.

Wameonesha umoja kupinga mashambulio ya juma lilopita yaliyofanywa na magaidi Waislamu.

Baada ya kusimama kimya kwa dakika moja familia za baadhi ya wanyonge 17 waliouwawa waliongoza mhadhara mmoja katika mji mkuu wa Ufaransa.

Viongozi kadha wa kimataifa walikamatana mikono na kujiunga na mhadhara mmoja.

Waziri Mkuu wa Utaliana, Matteo Renzi, aliiambia BBC, kwamba tukio la leo lilitoa ujumbe mzito:

Mie nina hakika kuwa watu hufanya historia.

Katika kisa hichi watu wa Paris, watu wa Ufaransa, lakini nafikiri watu wa Ulaya, wanatoa ujumbe wa uhuru wa kujieleza.

Ni kitu muhimu.

Mashambulio dhidi ya waandishi wa habari ni jambo baya.

Lakini matokeo yake ni matokeo ambayo yanaonesha wazi kuwa siku za mbele maadili yetu ndio yatayofuatwa, na kwamba sisi tuna nguvu zaidi kushinda vitisho na ugaidi.

Na kumefanywa maandamano makubwa katika miji mengine ya Ufaransa - kama Lyon, Bordeaux na Marseille.

Mjini Madrid, mamia ya Waislamu - waliobeba mabiramu yakisema 'siyo kwa niaba yetu' - waliandamana karibu na kituo cha treni ambako mwaka wa 2004, mabomu yalitegwa na wapiganaji Waislamu na kuuwa karibu watu mia-mbili.

Maelfu piya walikusanyika Brussels, Berlin na Vienna.

Mjini London mahali patatu pamewashwa taa za rangi za bendera ya Ufaransa, nyekundu, nyeupe, na buluu.

Maandamano piya yamefanywa Cairo, Sydney na Tokyo.