Ubani wa kutafuna wamtia matatani mtoto

Image caption Mtoto huyo inaarifiwa aliiba pakiti ya bigjii na kukosa kufika mahakamani mara mbili

Kiongozi mmoja wa mashitaka katika jimbo la Idaho nchini Marekani, alitoa kibali cha kukamatwa kwa mtoto mwenye umri wa miaka 9 ambaye alikosa kufika mahakamani kama alivyotakiwa.

Kituo kimoja cha televisheni nchini humo KHQ-TV kimeripoti kwamba mtoto huyo mvulana alifikishwa mahakamani kwa kuiba paketi ya gamu/bigiji/chingamu/ au ubani wa kutafuna .

Polisi wanasema kuwa ni mara ya kwanza kwa miaka 30 kwa kibali cha kukamatwa kutolewa kwa mtu mwenye umri mdogo kama huo.

Inaarifiwa mtoto huyo alikosa kufika mahakamani kwa sababu jamaa wake walikosa uwezo wa kumpeleka mahakamani humo na kwa sababu ya umri wake mdogo asingeweza kuendesha gari.

Hata hivyo mwendesha mkuu wa mashitaka Barry McHugh, alisema alilazimika kutoa kibali cha kukamatwa kwa mtoto huyo kwa sababu ni mara yake ya pili kukosa kufika mahakamani.

Hata hivyo alisema hawezi kuzungumzia tena kesi hio kwa sababu inamhusu mtu aliye chini ya umri wa miaka 18.

Mtoto huyo kwa sasa amezuiliwa katika kituo cha watoto wakorofi.