Juhudi za uokozi zashika kasi Malawi

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Serikali ya Malawi imetoa wito kwa jamii ya kimataifa iweze kuisaidia

Juhudi za kuwaokoa watu walioathiriwa na mafuriko katika sehemu kubwa ya Malawi imeanza kufuatia mafuriko mabaya kukumba nchi hio ambapo takriban watu 50 wamefariki tangu mvua kubwa kuanza kunyesha karibu mwezi mmoja uliopita.

Mafuriko hayo, yamesababisha watu 100,000 kuachwa bila makao.

Serikali imepeleka jeshi na vifaa kwa kutumia helikopta kujaribu kuwaokoa maelfu ya watu walionaswa katika baadhi ya maeneo ya nchi hio.

Idadi ya waliofariki huenda ikaongezeka hasa baada ya miili mingine minne kupatikana katika mto wa Shire ambao ulikuwa umefurika kusini mwa nchi.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Maelfu ya watu wameachwa bila makao baada ya nyumba zao kusombwa na maji

Inaarifiwa watu wengine wangali hawajulikani waliko. Lakini juhudi za uokozi pia zimetatizika kutokana na ukosefu wa barabara na uharibifu wa majengo katika wilaya 15 nchini Malawi.

Daraja pia zimeharibika baada ya kusombwa na maji na katika maeneo mengine maji yamefurika huku heklikopta zikikosa sehemu za kutua.

Katika nchi jirani ya Msumbiji, taarifa zinasema kwamba kikosi cha jeshi la Afrika Kusini kitapeleka wanajeshi kusaidia katika juhudi za uokozi.

Mafuriko yamewaua watu 25 na kuwaacha maelfu ya wengine bila makao.

Barabara moja kuu imeharibiwa huku sehemu nyingine za nchi zikikumbwa na giza baada ya mvua kuangusha milingonti ya stima.