Wakamatwa kwa kuwachoma wanaume 3

Image caption Polisi wa India wanashika doria katika maeneo yaliyoathiriwa na vurugu

Watu 14 wamekamatwa katika jimbo la Bihar Kaskazini mwa India baada ya kushukiwa kuwachoma moto watu watatu wakiwa hai pamoja na nyumba zao India na kusababidha ghasia Jumapili katika mtaa wa Ajitpur eneo la Muzaffarpur.

Inaarifiwa zilichochewa na kupatikana kwa mwili wa mwanamume wa kihindu katika kijiji hicho zaidi ya wiki moja baada ya mwanamume huyo kutoweka.

Afisaa mmoja wa polisi, aliambia BBC kwamba mwanamume huyo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na msichana muisilamu.

Inaarfiwa alitekwa nyara na kuuawa.

Umati mkubwa ulikusanyika katika eneo hilo baada ya mwili kupatikana na kuanza kuteketeza nyumba zaidi ya kumi huku watu watatu wakiuawa.

Hali katika eneo hilo ni mbaya ingawa polisi wameweza kuidhibiti.

Maafisa wanasema babake mwanamue huyo, aliwasilisha malalamiko kwa polisi huku akidai kuwa mwanawe alitekwa nyara.

Jimbo la Bihara limeamrisha kufanywa uchunguzi huku mamia ya polisi wakishika doria katika eneo hilo.

Idadi ya wahindu nchini India ni asilimia 80 ikilinganishwa na waisilamu ambao ni asilimia 14 ya watu bilioni 1.2 nchini humo.

Wadadisi wanasema jamii hizo huishi kwa amani lakini kuna nyakati fulani ambapo wao huvurugana.

Mnamo septemba mwaka jana takribna watu 50 walifariki katika vurugu kati ya wahindu na waisilamu katika eneo la Muzaffarnagar.