Matajiri kumiliki mali zaidi

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Warren Buffet mmoja wa matajiri wakubwa duniani

Shirika la kimataifa la misaada nchini Uingereza, Oxfam, limeonya kwamba kufikia mwaka ujao, matajiri ambao ni asilimia moja ya idadi ya watu duniani, watamiliki mali zaidi kuliko asilimia 99 iliyosalia ya watu.

Shirika hilo linataka kuongeza shinikzo kwa wanasiasa kukabiliana na suala la ukosefu wa usawa katika umiliki wa mali wakati viongozi wanajitayarisha kukutana nchini Switzerland wiki hii kwa kongamano la uchumi duniani.

Oxfam inasema kuna ongezeko kubwa la pengo kati ya utajiri na maskini.

Linasema umewadia wakati kwa viongozi duniani kuwajibika zaidi. Mkuu wa masuala ya nje wa shirika hilo, Katie Wright, amesema mojawapo ya mambo ambayo yanastahili kukabiliwa ni ukwepaji wa kulipa kodi.

Kwa mujibu wa shirika la Oxfam, mali ya matajiri walio wachache duniani iliongezeka kwa asilimia 48 mwaka jana kutoka asilimia 44 mnamo mwaka 2009.

Kupanuka kwa pengo kati ya maskini na matajiri duniani kumekuwa kizingiti katika vita dhidi ya umaskini kwani makampuni makubwa zaidi duniani yanashinikiza Marekani na Ulaya kushurutisha matajiri kulipa kodi kwani watu wanaolipa sana kodi ni wale wenye kipato cha kadri.

''Je tunataka kuishi katika dunia ambayo matajiri ambao ni asilimia 1 wanaomiliki mali nyingi kuliko watu wengi duniani?''alihoji afisaa mkuu mtendaji wa Oxfam alisema katika taarifa yake, Winnie Byanyima,

''Kiwango cha pengo kati ya maskini na matajiri duniani ni kubwa sana na licha ya swala hilo kuangaziwa, pengo hilo bado linaendelea kupanuka.''

''Wakati viongozi wa dunia kama vile Barack Obama na mkuu wa shirika la fedha duniani Christine Lagarde wamezungumza swala la kupunguza umaskini duniani, bado tunasubii viongozi watakaochukua hatua,''alisema Byanyima.

Taasisi za afya na za kifedha, zilitumia mamilioni ya dola kuishinikiza Marekani kuweka sheria nzuri mnamo mwaka 2013 na zaidi ya dola milioni 200 ilitumika jkusihinikiza Ulaya kubadilisha mambo.

Wakati huohuo, mmoja kati ya watu 9 hawana chakula na watu zaidi ya bilioni moja wanaishi kwa chini ya dola moja kwa siku, takwimu ambazo zinatoa tasiwra mbaya sana kwa matajiiri duniani.

Shirika la Oxfam linatoa wito kwa viongozi wa dunia kuhakikisha kwamba mashirka au kampuni za watu matajiri zinalipa kodi huku serikali zikiongeza shinikizo kuhakikisha kwamba watu maskini wanapata huduma za afya na elimu.