'Selfie' yamtia matatani Miss Lebanon

Haki miliki ya picha
Image caption Miss Lebaon katika mashindano ya Miss Universe mjini Miami Marekani

Uhusiano wa Lebanon na Israel umekuwa na panda shuka zake hadi wa leo, kwa hivyo ilipotokea picha ya 'selfie' ya mrembo wa Lebanon akiwa karibu na mwenzake wa Israel kwenye mitandao ya kijamii mambo bila shaka yakawa mabaya zaidi.

Doron Matalon, mwenye umri wa miaka ambaye kwa sasa ndiye Miss Israel, alipost picha yake kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram ikimuonyesha akiwa na mwenzake wa Lebanon Saly Greige pamoja na warembo wengine kutoka Japan na Slovania kwenye mashindano ya mwanamke mrembo zaidi duniani mjini Miami.

Picha hio tayari imeanza kumletea masaibu mrembo wa Lebabon

"hauwakilishi Lebanon," aliandika mtu mmoja kutoka Lebanon kwa lugha ya kiarabu kwenye Facebook.

''Ikiwa utauza thamani yako basi ni kama kuiuza nchi yako,'' alitweet mtu mwingineo kutoka Lebanon.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Picha ya Miss Israel aliyojipiga na Miss Lebanon imemuingiza kikaangoni Miss Lebaon

Mrembo huyo wa Lebanon alikosolewa sana kwenye mitandao ya kijamii ingawa alijitetea akisema kuwa yeye alikuwa anapiga picha na warembo wengine kutoka Japan na Slovenia wakati Miss Israel alipojiunga nao bila ya wao kujua na kupiga ile picha ya Selfie akiwa nao.

Hata hivyo mashabiki wa Lebabon walimtetea Miss Lebanon wakisema, ''hilo ni shindano tu la warembo wala sio vita vya mataifa. Kwa hivyo badala ya kumkaripia Miss Lebanon wamuunge mkono, '' aliandika mwanamke mmoja

Lakini watu wengi hawakupenda matamshi yake.

"jamani kwanini tusingumzie amani na kuondoa siasa katika mambo mengi tunayoyafanya? Ninasikitishwa sana na hilo, ndio imenibidi kuandika haya, '' aliandika myahudi mmoja.

Naye Miss Israel aliamua kuandika katika ukurasa wake wa Facebook: '' mimi haya hayanishangazi lakini bado yananipa huzuni. Inasikitisha kwamba hatuwezi kuondoa siasa na ukali wa maneno hata katika tamasha la urembo, kwa wiki kadhaa tu ambapo tunakutana na wasichana wengine kutoka nchi mbali mbali na pia kutoka nchi jirani,''

''Hakuna cha ajabu kuhusu watu walivyoichukulia picha yenye utata ya Miss Lebanon kwani ni kitu kilichotarajiwa,'' alisema mwandishi mmoja wa Lebanon ambaye pia ni mwanaharakati wa haki za wanawake, Jumana. ''Daima tuko vitani na Israel, sio vyema kupiga picha na wale wanaoonekana kama maadui wako mkionekana mkicheka,'' alisema Jumana.

Lakini wengi wa walebanon walishangaa sana kwa nini Miss Lebanon alikaripiwa kwa kuonekana akiwa katika picha na mwenzake wa Israel wakati hali hio haikujitokeza waziri mkuu wa Israel Benajamin Netanyahu alipoonekana akiwa na waziri na mambo ya kigeni wa Lebanon katika maandamano mjini Paris.