Jeshi la DRC kuwakabili waasi wa kihutu

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wanajeshi wa DRC

Mkuu wa majeshi katika jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, ametangaza operesheni kali ya kikosi cha Congo kikishirikiana na Umoja wa mataifa dhidi ya kundi la wapiganaji wa waasi wa kihutu wa Rwanda.

Hii ni hatua iliyosubiriwa kwa muda tangu makataa ya mwisho kutolewa mnamo januari mbili mwaka huu na jumuiya ya kimataifa kwa waasi kusalimu amri na kurejesha silaha au mashambulio makali dhidi yake yaanzishwe.

Maafisa wa Umoja wa mataifa walioko DR Congo, wamesema kuwa operesheni hiyo bado haijaanza.

Jenerali Alberto Dos Santos Cruz, ameiambia BBC kuwa wanaandaa kila kitu tayari ndiposa waanze kuwakabili waasi.

Kwa mjibu wa jenerali Cruz, mianya yote ya kutorokea waasi hao imezibwa na wanajeshi wa Congo huku walinda usalama wa umoja wa mataifa wakitoa usaidizi wa silaha na vifaa vinginevyo.

Awali katika ushirikiano kama huo, umoja wa mataifa ulisaidia kutoa saada wa vifaa, kama vile ndege za kivita na usambazaji wa vyakula, ilihali jeshi la Congo likiwa katika mstari wa mbele katika kukabiliana na waasi.

Image caption Waasi wa kihutu FDLR

Kundi hilo la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda-DFLR linakisiwa kuwa na wanajeshi elfu moja mia tano waliotawanyika katika maeneo ya vijijini na kujumuika na raia, na itakuwa vigumu zaidi kukabiliana nalo kuliko lile kundi la M23.

Kundi ambalo jeshi la Congo likisaidiwa na walinda usalama wa umoja wa mataifa walipigana nao mwaka 2013.

Kundi la FDLR limesema kuwa halitajitetea katika vita hivyo, lakini linataka kujadiliana na serikali ya Rwanda mjini Kigali, inayolilaumu kwa kuhusika katika mauaji makubwa ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994.