Netanyahu: walioua wanajeshi watakiona

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Benjamini Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel

Waziri Mkuu wa Israel Benjamini Netanyahu amesema wote waliohusika na mashambulizi dhidi ya msafara wa majeshi ya Israel watalipa gharama ya waliyoyafanya.

Israel imesema wanajeshi wake wawili waliuawa na wengine saba kujeruhiwa katika shambulio lililotekelezwa na Hezbollah katika mpaka kati ya Lebanon na Israel.

Mara tu baada ya shambulio lililosababisha wanajeshi wawili kuuawa,Israel ilijibu mapigo kwa kufyatua makombora kwenda Lebanon.

Nayo majeshi ya Kulinda amani ya Umoja wa mataifa nchini Lebanon limesema mwanajeshi wao mmoja aliuawa.

Akitoa onyo dhidi ya waliohusika na shambulizi hilo Netanyau amesema wote waliohusika lazima wawajibike.

"Yeyote aliyehusikia na shambulizi atalipa gharama. Kwa nyakati fulani Iran kupitia Hezbollah imekuwa ikijaribu kuanzisha mashambulizi ya kigaidi dhidi yetu kutoka katika milima ya Golan. Tutajibu kwa nguvu zetu zote majaribio ya mashambulizi haya,'' alisema Netanyahu.

''Kwa matukio yote haya mpango wetu ni kulilinda taifa la Israel. Tunachozingatia ni usalama wa taifa la Israel na watu wake. Ndio maana tutachukua hatua na tataendelea kuchukua hatua."Amesema Netanyahu.

Nayo Hezbollah kwa upande wake limekiri kufanya shambulio hilo kwenye msafara wa majeshi ya Israel kwenye mpaka kati ya Lebanon na Israel.

Hezbollah imesema shambulio hilo ni majibu ya mashambulizi ya angani yaliyofanywa na Israel siku kumi zilizopita ambayo yaliua Jenerali wa Iran na wapiganaji sita wa Hezbollah katika mji wa Queneitra nchini Syria.

Msemaji wa Hamas huko Gaza Sami Abu Zuhria mesema shumbulio hilo dhidi ya Israel lilikuwa la haki.