Afcon:Ivory Coast yawang'oa Algeria 3-1

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wachezaji wa timu ya Ivory Coast waishangilia ushindi katika michezo ya Kombe la Mataifa ya Afrika inayoendelea Equatorial Guinea

Wilfried Bony aliifungia mara mbili Ivory Coast na kuivusha hadi nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika, pale timu yake ilipopambana na Algeria katika mchezo wa pili wa robo fainali, Jumapili.

Mshambuliaji huyo mpya wa Manchester City aliifungia timu yake bao la kwanza kwa kichwa kufuatia krosi iliyochongwa na Max Gradel katika dakika ya 26 ya mchezo.

Hilal Soudani aliisawazishia Algeria katika dakika ya 51 na baadaye kumlazimisha mlinda mlango wa Ivory Coast Sylvain Gbohouo.

Kazi nzuri ya Gbohouo ilijibiwa na bao la pili la Bony ambaye alitumia vema mpira wa adhabu uliopigwa na Yaya Toure kufunga tena kwa kichwa. Gervinho alihitimisha kichapo cha Ivory Coast kwa Algeria pale alipofunga goli la tatu katika dakika ya 90 na kuzima kabisa ndoto za Algeria kucheza nusu fainali za michuano hiyo.

Katika mchezo wa kwanza Ghana iliirarua Guinea kwa kuichabanga magoli 3-0. Cristian Atsu aliifungia Ghana mabao 2 na Kwesi Appiah akifunga moja.

Kwa matokeo hayo, sasa Ivory Coast itapambana na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Jumatano, huku Ghana ikivaana na wenyeji Equatorial Guinea Alhamisi.