Yanga yaongoza ligi Tanzania Bara

Haki miliki ya picha bbc
Image caption Vijana wa Jangwani wakiwajibika

Bao lililofungwa na nahodha Nadir Haroub “Cannavaro” lilitosha kuipa Yanga ushindi wa goli 1-0 dhidi ya wenyeji wao, Coastal Union katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyomalizika mkoani Tanga, Kaskazini mwa Tanzania.

Cannavaro alifunga goli hilo dakika 11 ya kipindi cha kwanza kwa kichwa akiunganisha nyavuni mpira uliorushwa na beki Mbuyu Twite.

“Ni furaha kupata ushindi wa ugenini na kupata pointi tatu muhimu zinazotuwezesha kuongoza ligi”, alinukuliwa Cannavaro akiongea muda mchache baada ya mechi hiyo iliyokuwa ya vuta nikuvute.

Wenyeji, licha ya kufungwa walicheza mpira wa ushindani na walipata nafasi kadhaa za kufunga ila walizipoteza

Kwa mfano, Hussein Swedi alikosa goli, ambalo lingeweza kubadilisha matokeo ya kuwa 1-1 dakika 8 kabla ya mechi kumalizika pale aliposhindwa kuunganisha wavuni mpira uliopigwa na Godfrey Wambura wakati mabeki wa Yanga walipozubaa wakidhani Swedi kaotea.

Ushindi huo unaifanya Yanga iongoze ligi ikiwa na pointi 22 ikifuatiwa na timu ya Azam ikiwa na pointi 21.

Mara ya mwisho, Yanga ililazimishwa droo ya 0-0 na timu ngeni katika ligi, Ndanda FC katika mechi iliyochezwa uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.