Jordan yaapa kupambana na Islamic State

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mfalme Abdullah wa Jordan

Mfalme wa Jordan ameahidi mapambano yasiyo na huruma dhidi ya wapiganaji wa Islamic State kufuatia kuuawa kwa rubani wa nchi hiyo.

Baada ya mkutano wa makamanda wa juu wa jeshi na maafisa usalama, Mfalme Abdullah amesema vita hivyo vitaelekezwa dhidi ya kundi hilo na damu ya rubani huyo wa ndege za kivita Muath al-Kasasbeh haitapotea bure.

Hapo jana, Jordan iliwanyonga wafungwa wawili wapiganaji wenye msimamo mkali waliokuwa katika orodha ya adhabu ya kifo, kama kulipiza kisasi cha kuuawa kwa rubani wake huyo.

Miongoni wa walionyongwa ni Sajida Al-Rishawi, ambaye wapiganaji wa Islamic State walitaka aachiwe kama sehemu ya kubadilisha na mateka huyo wa Jordan waliokuwa wakimshikilia.

Katika hatua nyingine kundi la wabunge wa Uingereza limeitaka nchi yao kuchukua hatua zaidi kupambana na kundi hilo la Islamic State.

Ripoti kali iliyotolewa na kamati ya Ulinzi ya bunge hilo imesema maafisa na maafisa waandamizi wa jeshi wameshindwa kuanzisha mikakati iliyowazi kufikia malengo ya kuwashinda wapiganaji hao wenye msimamo mkali.

Awali serikali ya Uingereza ilisema hatua zinazochukuliwa za kutoa msaada wa kijeshi ni moja ya sehemu ya mikakati ya ulimwengu kupambana na kundi hilo.