UK yalaumiwa Operesheni dhidi ya IS

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wanamgambo wa Islamic State nchini Iraq

Wito umetolewa kwa Uingereza kuongeza nguvu za kupambana na Wanamgambo wa Islamic State.

Kamati ya kuteuliwa ya maswala ya Ulinzi ndani ya Bunge hilo imesema Uingereza imeshiriki asilimia 6 tu ya mashambulizi ya anga dhidi ya kundi hilo la Jihad na kusema kuwa wanashangazwa kwa kuwa haifanyi jitihada za hali ya juu.

Wabunge wamesema Wanamgambo hawa wamejiimarisha sehemu za nchi ya Iraq na Syria .

IS imekuwa ikishikilia maeneo mengi na imekuwa ikijihusisha na vitendo vya kikatili ikiwemo kukata vichwa vya Mateka Raia wa Uingereza.

Ripoti inasema kuwa IS kujitokeza kutoka eneo la Mashariki ya kati ni tishio kwa usalama wa Dunia.

Serikali ya Uingereza imelaumiwa kwa kutokuwa na mbinu za kijeshi.

Ndege za kijeshi zilianza kupeleka Wanajeshi wake nchini Iraq mwezi Septemba baada ya Wabunge kuunga mkono Operesheni za kijeshi dhidi ya Wanamgambo wa IS nchini Iraq.

Hata hivyo, Bunge halikuombwa kupiga kura kuunga mkono mpango wa Operesheni za kijeshi dhidi ya IS nchini Syria.

Kamati ilifanya ziara nchini Iraq Mwezi Desemba na kubaini kuwa kulikuwa na Wanajeshi watatu pekee nje ya Miji ya kikurdi, ikilinganishwa na Wanajeshi 400 wa Australia, 280 wa Italia na 300 wa Uhispania.

Ripoti hiyo imeitaka Serikali ya Uingereza kufanya tathimini ya hali ilivyo nchini Iraq kisha kutoa msaada kwa vikosi vya usalama vya Iraq na Wapiganaji wa Peshmerga watakapokuwa tayari kwa mapigano dhidi ya IS.