APC yalaani kuakhirisha uchaguzi Nigeria

Professor Attahiru Jega, mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Nigeria

Chama kikuu cha upinzani cha Nigeria kimelaani kuakhirishwa kwa uchaguzi uliokuwa ufanywe juma lijalo, na sasa kucheleweshwa hadi mwisho wa mwezi March.

Chama cha APC kimesema kuwa jeshi limetaka uchaguzi uakhirishwe ili kusaidia kampeni ya Rais Goodluck Jonathan.

Mjumbe wa senate wa chama cha APC, Lawali Shuaibu, aliiambia BBC, tishio la mashambulio ya Boko Haram siyo sababu pekee ya kuakhirisha uchaguzi:

"Hatujui hasa kwanini umeakhirishwa.

Sababu waliyotoa ya kuakhirisha uchaguzi kwa wiki sita ni ya hali ya usalama.

Tunajiuliza, kitu gani kitatokea katika wiki sita zijazo ambacho kisingeweza kutokea katika miaka sita iliyopita.

Sisi tunahisi kuna sababu nyengine, siyo tu usalama."