CAF yapongeza michuano ya AFCON 2015

Image caption Nahodha wa Ivory Coast Yaya Toure mwenye jezi rangi ya machungwa akisubiri kupokea kombe kutoka kwa rais Nguema wa Equitorial Guinea mwenye skafu shingoni, wakati Ivory Coast ilipoifunga Ghana kwa Penalti 9-8 Jumapili.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu, barani Afrika, amezielezea Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zilizofanyika nchini Equatorial Guinea kuwa "maajabu"

Mwezi Novemba pekee, wenyeji wa awali, Morocco iliomba michuano hiyo icheleweshwe, lakini ombi hilo lilikataliwa, na kusababisha ihamishwe.

Licha ya ghasia na huduma duni, Hicham el Amrani ameeleza kuwa yalikuwa mashindano yenye mafanikio.

"Kwa kuzingatia muda tuliokuwa nao, na mazingira yaliyokuwepo, kilichotokea kwa namna ilivyotokea yalikuwa maajabu - hakuna kilichokosekana," ameiambia BBC Sport.

"Tuna furaha juu ya maandalizi yote kwa ujumla, kwa muda tuliokuwa nao na raslimali tulizokuwa nazo, na nafikiri kilikuwa kitu amabcho tuliweza kuwa na michuano ambayo imemalizika vizuri."

Hata hivyo, mashindano hayo yaliyomalizika Jumapili kwa Ivory Coast kuishinda Ghana kwa mikwaju ya penalti baada ya kutofungana dakika 120 za mchezo na kunyakua kombe, yatakumbukwa kuwa mashindano yenye utata na magumu.

Ghasia zilitawala nusu fainali kati ya wenyeji na Ghana, wakati mchezo ulipovurugika kwa dakika 30 wakati chupa za maji zikirushwa uwanjani kutoka katika majukwa ya watazamaji, na kuwalazimisha mashabiki wa Ghaba, Black Starskujikusanya katikati ya uwanja nyuma ya goli ili kuokoa maisha yao.

Image caption Uwanja wa Bata wa mpira wa miguu uliofanyikia mchezo wa mwisho wa fainali za Afcon 2015 nchini Equatorial Guinea.

Helikopta ya polisi ilitumika kujaribu kurejesha hali ya amani wakati mashabiki wa Equatorial Guinea walipofanya fujo.

Na kulikuwa na utata mkubwa kuhusu penalti iliyopewa Equatorial Guinea dhidi ya Tunisia katika hatua ya robo fainali, ambapo wachezaji wa Tunisia walitakiwa kujizuia na ghasia walipomkimbiza mwamuzi wa mchezo huo Rajindraparsad Seechurn mwishoni mwa mchezo.

Rais wa chama cha soka cha Tunisia Wadie Jary amesimamishwa kujihusisha na shughuli zinazohusiana na Caf na Tunisia lazima iombe msamaha kwa Caf kufikia tarehe 31 Marchi kwa kuishutumu Caf kuhusu udanganyifu na isipofanya hivyo ifungiwe katika mashindano ya mwaka 2017.

Caf pia imemfungia Seechurn kwa miezi sita "kwa ufanisi mbovu" katika mechi hiyo.