Wakamatwa kwa tuhuma za ugaidi Sydney

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Tony Abbot waziri mkuu wa Australia

Polisi katika mji wa Sydney nchini Australia wamewafungulia mashitaka watu wawili wakipanga kufanya shambulio la kigaidi.

Watu hao wenye umri wa miaka 24 na 25, walikamatwa katika msako katika kitongoji cha magharibi mwa mji wa Fairfield Jumanne.

Taarifa za kula njama ya kufanya shambulio hilo bado hazijafahamika, lakini polisi wanasema kisu, bendera ya kikundi cha Islamic State (IS) na video ikielezea shambulio, vilikamatwa.

Australia, ambayo imejiunga na majeshi ya washirika kupambana na IS nchini Iraq, mwaka jana ilitoa tahadhari ya usalama nchini humo.

Hatua hiyo ilikuwa kuitikia kuongezeka kwa wasiwasi juu ya hali ya usalama nchini Iraq na Syria kuhusu madhara ya mgogoro wa makundi ya wapiganaji katika nchi hizo.

Mji wa Sydney nako uko katika hali ya tahadhari baada ya shambulio lililofanyika katika mgahawa mmoja mjini humo mwezi Desemba mwaka jana ambapo watu wawili walioshikiliwa mateka na mtu mwenye silaha kuuawa.

Waziri Mkuu Tony Abbott amesema kukamatwa kwa watu hao ni ishara kwamba IS inaendesha shughuli zake za uhalifu duniani kote, ikiwa ni pamoja na hapa Australia, na kwa masikitiko kuna watu nchini humu ambao wanahusika na uchochezi huu wa msimamo mkali na hata ugaidi".

Naibu Kamishna wa Polisi wa New South Wales Catherine Burn anaamini watu waliokamatwa Jumanne walikuwa wakijiandaa kufanya shambulio siku hiyo.

Video ilikutwa katika nyumba iliyofanyiwa upekuzi "ikimwonyesha mtu akisema juu ya kufanya shambulio", amesema DC Burn, akisema kukamatwa kwa watu hao ni "kielelezo cha kitisho"mashirika ya usalama sasa lazima yakabiliane na kitisho hicho.

Watu hao wawili, wametajwa katika mashitaka ya mahakama kuwa ni Omar Al-Kutobi na Mohammad Kiad, awali hawakutambuliwa na polisi na maafisa wa kupambana na ugaidi waliwatambua wakati walipopata taarifa juu yao Jumanne, na kuwafanya washughulikie tatizo hilo haraka, amesema.

Wameshitakiwa kwa kushiriki vitendo vya maandalizi au kupanga kitendo cha kigaidi. Walichagua kutofika kusomewa mashitaka ya awali, ambapo walinyimwa dhamana.