Watu 20 wauawa mgogoro wa Ukraine

Image caption Watu wapatao wawili waliuawa wakati basi kituo cha basi katika mji wa Donetsk kilipopigwa kwa kombora

Zaidi ya watu 20 wamekufa katika vurugu mashariki mwa Ukraine wakati viongozi wa Urusi, Ukraine, Ufaransa na Ujerumani wakijiandaa kwa mazungumzo ya amani ya Ukraine.

Askari kumi na tisa wa Ukraine wameuawa, wengi wao katika mji wa waasi wanaoungwa mkono na Urusi ambao wamesema wameuzingira mji huo.

Watu watano wameripotiwa kuuawa kwa mabomu katika eneo linalodhibitiwa na waasi katika mji wa Donetsk.

Wasuluhishi nchini Belarus bado wanajaribu kupunguza tofauti zilizopo kuelekea katika mkutano wa viongozi wa kutafuta amani ya Ukraine unaofanyika Jumatano.

Ukraine na mataifa ya magharibi yanaishutumu Urusi kwa kupeleka majeshi yake na silaha kuwasaidia waasi, lakini Urusi imekuwa ikikana shutuma hizi.

Mkutano wa viongozi unaofanyika katika mji mkuu wa Belarus, Minsk unatarajiwa kujikita katika kusitisha mapigano na kuondolewa kwa silaha nzito, ikiwa ni pamoja na kuunda ukanda usio na harakati za kijeshi.

Mwandishi wa BBC wa masuala ya diplomasia Bridget Kendall amesema bado haifahamiki ni kwa namna gani Rais Putin atajiandaa kutoa maelezo ya mgogoro huo wakati anaendelea kukana kuhusika kwa Urusi na vita nchini Ukraine.