Mipira mikubwa ya kondomu yalaumiwa Thai

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Afisa wa kampuni ya kutengeza mipira ya kondomu katika ufalme wa Thai akagua mipira hiyo

Maafisa wa afya katika ufalme wa Thai wamesema kuwa wavulana ambao wanaogopa kuchagua mipira ya kondomu zinazowatosha vizuri ndio chanzo cha mlipuko wa magonjwa ya zinaa miongoni mwa vijana.

Katika taarifa ilioambatana na siku ya wapendanao ya Valentine-siku ambayo maafisa wa Thai utoa onyo kuhusu mapenzi ya ujana, wizara ya afya ya uma ilionya kuwa magonjwa ya zinaa miongoni mwa wavulana wa miaka 10 hadi19 yameongezeka mara tano zaidi katika kipindi cha miaka 10 iliopita.

''Ni kwa sababu ni asilimia 43 ya vijana ndio wanaotumia mipira ya kondomu na kwamba huchagua mipira ambayo ni mikubwa ikilinganishwa na vipimo vyao huku wakiogopa kwamba watafanyiwa masikhara kwa kuwa wadogo''.

Wizara hiyo imeongezea kwamba inapanga kutumia dola millioni 1.4 mwaka huu ili kugawanya zaidi ya mipira millioni 43 kwa watu wote katika ufalme huo.

Vijana katika ufalme huo hufunzwa kutofanya ngono badala kuambiwa watumie kinga wakati wanapotekeleza tendo hilo.