Uchunguzi kifo cha Monson kuanza Mombasa

Haki miliki ya picha INTERNET
Image caption Mji wa Mombasa pwani ya Kenya ambako uchunguzi wa kifo cha Mwingereza Alexander Monson unatarajiwa kuanza leo Jumatatu.

Uchunguzi wa umma kuhusu kiini cha kifo cha Mwingereza Alexander Monson unatarajiwa kuanza Jumatatu Kisiwani Mombasa nchini Kenya.

Alexander Monson aliaga dunia akiwa hospitalini, baada ya kumamatwa na kupata majeraha akiwa mikononi mwa Polisi, huku polisi wakikana kuhusika.

Alexander Monson alikamatwa mnamo mwezi Mei mwaka 2012 kwa tuhuma za kupatikana na bangi. Siku iliyofuata kijana huyo alikufa hospitalini, huku mikono ikiwa imefungwa pingu kitandani.

Polisi wa Kenya wamesema kuwa marehemu alikufa baada ya kutumia madawa ya kulevya kupindukia.

Lakini uchunguzi wa madaktari umebainisha kuwa kifo chake Alexander kilisababishwa na jeraha la kichwa alilopata akiwa mikononi mwa Polisi.

Familia yake imekuwa ikitafuta haki bila mafanikio huku polisi wakisisitiza kuwa hakuna afisa aliyehusika na kifo chake.

Mkurugenzi wa mashtaka hatimaye aliagiza uchunguzi wa umma kufanyika ili ukweli upatikane. Lakini Nicholas Monson, baba yake marehemu, anasema hana matumaini makubwa kuwa ukweli utadhihirika.

Kwenye taarifa aliyochapisha katika gazeti la Uingereza la The Telegraph, Lord Monson ameeleza masikitiko yake kuwa jitihada zake kufanya kazi na viongozi wa Kenya zimegonga mwamba, baada ya serikali kukataa kubadili msimamo wake kuhusu kilichomuua Alexander.

Aidha Lord Monson amedokeza kuwa anamshuku mtu fulani kuwa ndiye alimuua mwanaye, na anatarajia kuonana naye ana kwa ana mahakamani Mombasa.

Jumla ya watu 56 wanatarajiwa kutoa ushahidi.